| Mnyika ataka uongozi wizarani ung’olewe |
MBUNGE
wa Ubungo (Chadema) John Mnyika ameitaka serikali kufanya mabadiliko
ya kimuundo na kiuongozi katika Wizara ya Nishati na Madini kwa
sababu imeshindwa kuhimili mahitaji katika sekta ya umeme, mafuta,
madini na gesi asilia.
Mnyika aliyasema hayo jana kupitia taarifa yake aliyoituma kwa vyombo vya habari.Alisema kutokana na Wizara ya Nishati na Mdini kushindwa kusimamia na kuhimili sekta zinazosimamiwa na Wizara hiyo umefika wakati wa kufanyika kwa mabadiliko ya kimiundo ndani ya Wizara. Alisema Disemba 8, mwaka jana Wizara ya Nishati na Madini ilitoa taarifa kwa umma kuhusu maendeleo ya sekta ya Nishati na Madini na kufuatia taarifa hiyo tarehe Disemba 14, mwaka jana nilitoa tamko la kueleza kushangazwa na ukimya wa serikali kuhusu haja ya kutoa taarifa kwa umma ya utekelezaji wa mpango wa umeme wa dharura. “Iwapo Wizara ingekuchukua hatua thabiti tangu wakati huo, kusingetokea kwa tatizo la mgao wa umeme wa mara kwa mara. “Ikumbukwe kwamba mpango wa dharura ulipowasilishwa bungeni Agosti 13, mwaka jana serikali ilieleza kuwa imepanga kuongeza MW 572 ifikapo Disemba, mwaka jana, kati ya hizo, MW 150 ilikuwa zizalishwe kupitia makubaliano baina ya Shirika la Hifadhi ya Jamii (NSSF) na Tanesco jambo ambalo mpaka sasa halijatekelezwa ipasavyo,” alisema. Alisema jambo hilo linatia mashaka zaidi utendaji wa Wizara ya Nishati na Madini kwa kuwa mpaka sasa Tanesco haijapata mkopo wa Sh408 bilioni kutoka katika benki kwa ajili ya kuendesha mitambo ya dharura ya IPTL, Symbion, Aggreko na kulipia madeni mengine kutokana na kutokamilisha masharti muhimu ikiwamo ya kupata dhamana kutoka kwa serikali. Mnyika alisema udhaifu wa kutokutekeleza mipango ya uzalishaji wa gesi na makaa ya mawe kwa wakati, umesababisha utegemezi mkubwa kwenye matumizi ya mafuta katika mitambo ya kuzalisha umeme wa dharura. “Zaidi ya nusu ya umeme unaozalishwa nchini hivi sasa ambao ni sawa na MW 660, unazalishwa kwa kutumia dizeli, mafuta ya ndege na mafuta mazito ambayo yanaagizwa kutoka nje ya nchi. “Hii imesababisha mahitaji makubwa ya fedha za kigeni kwa ajili ya kuagiza mafuta na kusababisha kuporomoka kwa thamani ya shilingi. Pia uagizaji huo umeathiri urari wa biashara na mfumuko wa bei na kusabaisha Watanzania kuwa na maisha magumu,” alisema. Mnyika alifafanua kwamba pamoja na kuwa na ahadi za mpango wa dharura, bado hazijatekelezwa kwa ukamilifu na kwamba serikali inaendelea kutumia zaidi ya Sh2 bilioni kila siku kwa ajili ya kununua mafuta ya kuzalishia umeme.Alisema matumizi hayo yanapaswa kufanyiwa uchunguzi wa kina kuhusu vyanzo vya fedha hizo na uhalali wa matumizi ya miradi ya Aggreko International, Symbion Power LLC na IPTL. “Katika hali hii, hatua za haraka zinapaswa kuchukuliwa za kuitaka Wizara ya Nishati na Madini kutoa taarifa ya kina kwa umma kuhusu hali halisi ya utekelezaji wa mpango wa umeme wa dharura pamoja na kudhibiti mianya ya ubadhirifu ambayo imeanza kujitokeza,” alisema |
0 Comments