CCM wachuana ubunge Afrika Mashariki

MAKADA 42 wa CCM wanatarajiwa kuchuana kuwania nafasi nane za ubunge katika Bunge la Afrika Mashariki (EALA), baada ya jana kuteuliwa na Kamati Kuu (CC) ya Halmashauri Kuu ya Taifa (NEC), ya chama hicho huku wengine 22 wakitupwa nje ya kinyang’anyiro.
Katika kinyang’anyiro hicho, jumla ya wanachama 64 waliomba ridhaa ya chama kuwania nafasi hizo, akiwemo Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Mara Makongoro Nyerere, Meya wa zamani wa Jiji la Dar es Salaam, Adam Kimbisa na Katibu wa UVCCM Mkoa wa Arusha,  Mrisho Gambo ambao wote wameshinda.
WanaCCM  maarufu walioshindwa katika kinyang’anyiro hicho ni pamoja na Mwenyekiti wa UVCCM Mkoa wa Arusha,  James Ole Millya na mbunge wa zamani wa Kibaha Mjini, Dk Zainab Gama.
Akizungumza na waandishi wa habari Dares Salaam jana, Katibu wa Itikadi na Uenezi wa CCM, Nape Nnauye alisema wagombea hao watapigiwa kura na wabunge wa CCM Mjini Dodoma Aprili 3, mwaka huu na kubaki 24.
Alisema kura hizo za wabunge wa CCM zitasimamiwa na Mjumbe wa Kamati Kuu, Abdulrahman Kinana, Makamu Mwenyekiti wa Jumuiya ya Wazazi ya chama hicho, Dogo Mabruki pamoja na Nape mwenyewe.

“CCM ina nafasi nane za ubunge wa Afrika Mashariki, hawa 24 watachuana ili kuwania nafasi nane,” alisema.
Aliwataja wengine waliopita katika hatua hiyo ya kwanza kwa kundi la wanaume kutoka bara kwamba ni  Dk Aman Kabourou ambaye alikuwa Mbunge wa Afrika Mashariki, kwa tiketi ya CCM, John Ngongolo, Dk Evans Rweikiza, Siraju Kaboyonga ambaye aliwahi kuwa Mbunge wa Tabora Mjini, Bernard Murunya, Dk Edmond Mndolwa, Christopher Awinia na Dk Hilderbrand Shayo.

Wengine ni Handley Mafwega, William Malecela, Mussa Mnyeti, Elibariki Kingu, Simon Berege na Godfrey Mosha. Katika kundi hilo, waliojitokeza walikuwa 45 na waliopendekezwa walikuwa 17.
Waliopitishwa kwa upande wa wanawake kwa Tanzania Bara ni Janeth Mmari, Janet Mbene, Fancy Nkuhi, Norah Mukami, Shally Raymond, Shy-Rose Bhanji, Ngollo Malenya, Godbertha Kinyondo, Hamidah Kalua, Angela Kizigha, Happyness Lugiko na Ruth Msafiri… “Katika kundi hili la wanawake, waliojitokeza walikuwa 17 lakini waliopendekezwa walikuwa 12.”
Alisema  kwa upande wa Zanzibar, wanaume waliopitishwa ni Dk Said Bilal, Abdallah Mwinyi, Dk Haji Haji, Dk Ahmada Khatib, Zubeir Maulid, Khamis Makame, Abdul Aziz Salim na Mbwana Mwinyi.
“Kwa wanawake ni Septuu Nassor, Safia Rijaal, Rukia Msellem, Sabah Ali na Maryam Yahaya,” alisema Nape.
Akizungumzia kinyang’anyiro hicho, Nape alisema kimethibitisha kwamba CCM hakijaishiwa sera kama baadhi ya wapinzani wake wanavyodai kwa kuwa kimewashirikisha wagombea wengi wasomi.

“Wanaosema CCM imefulia hapa wataishiwa la kusema kwa kuwa idadi kubwa ya waliojitokeza ni madaktari na maprofesa, hii inaonyesha jinsi chama kilivyo na nguvu na kupendwa na watu,” alijigamba.
Ubunge miaka sita
Kwa mujibu wa kanuni za Bunge la Afrika Mashariki,  wanaochaguliwa huwakilisha nchi zao kwa miaka sita.
Waliochaguliwa mwaka 2006 walianza kazi mwaka 2007 na wanamaliza muda wao mwaka huu huku wanaochaguliwa wakati huu, wataanza kazi hiyo mwaka 2013 na wanatarajiwa kumaliza kipindi chao mwaka 2018.
Wabunge waliokuwa kwenye Bunge linalomaliza  muda wake ni Dk George Nangale, Abdullah Mwinyi, Kate Kamba, Dk  Kabourou, Fortunatus Masha, Dk Didas Massaburi, Bilal na Sebtuu Nassor.

Katibu wa Bunge, Dk Thomas Kashilila alisema hivi karibuni kwamba uchaguzi wa wajumbe tisa watakaoiwakilisha Tanzania katika Bunge hilo la EALA utafanywa na wabunge wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wakati wa Mkutano wake wa Saba utakaofanyika Dodoma, kuanzia Aprili 10 hadi 20, mwaka huu.
Alisema uchaguzi huo unafanyika kwa kuzingatia kuwa muda wa Bunge hilo lililoingia madarakani mwaka 2006, utafikia ukomo wake Juni 4, 2012.
Kwa mujibu wa kanuni, Katibu wa Bunge ndiye Msimamizi wa Uchaguzi huo na atapaswa kutoa tangazo kwenye Gazeti la Serikali kwa mujibu wa masharti yanayohusika, kuhusu siku ya uteuzi, ambayo ni Aprili 10 na siku ya uchaguzi, Aprili  17.
Katika Tangazo hilo, Katibu wa Bunge pia atatoa masharti yanayopaswa kuzingatiwa na wagombea wa vyama vyote vya siasa vyenye uwakilishi bungeni kuhusiana na uchaguzi huo kwa ajili ya kuviwezesha kuanza mchakato wa kuwapata wagombea kupitia vyama hivyo ambao majina yao yatawasilishwa bungeni kwa ajili ya kupigiwa kura