| Mnyika: Tunataka maelezo ya utafutaji, uchimbaji urani |
| |
| MBUNGE
wa Jimbo la Ubungo (Chadema) , John Mnyika ameitaka Wizara ya Nishati
na Madini, kutoa maelezo juu ya hatua iliyofikiwa katika kuboresha
mfumo wa Sera, Sheria, Kanuni na Taasisi kuhusu Utafutaji na Uchimbaji
wa madini ya urani. Mnyika aliyasema hayo jijini Dar es Salaam jana , ambapo aliitaka Wizara hiyo ieleze hatua ambazo zimefikiwa kwa kushirikiana na vyombo vingine vya serikali ikiwamo Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) ili kuhakikisha umiliki, manufaa na usalama unakuwapo kwa madini hayo. . “Ni vyema Wizara ikatoa maelezo juu ya hatua ambazo imefikia kuhusu mauzo na mabadilishano ya umiliki yaliyofanyika baina ya Kampuni ya Australia (Mantra Resources) na Kampuni ya Urusi ya ARMZ Uranium Holding kampuni tanzu ya Rosato katika hatua ambazo zimefikiwa katika uchimbaji wa madini ya Urani,” alisema Mnyika na kuongeza . “Itakumbukwa kwamba kwa nafasi yangu ya Uwaziri Kivuli wa Nishati na Madini nilieleza masikitiko yetu juu ya maamuzi ya serikali ya kuendelea na hatua za mbele katika utafutaji na uchimbaji wa madini ya urani bila kukamilisha maandalizi ya kisera, kisheria, kikanuni na kitaasisi kama nilivyo hoji Bungeni Julai 15 mwaka jana,” alisema. Alisema suala hilo la Uchimbaji wa Urani linahitaji umakini wa hali ya juu la sivyo linaweza kusababisha upotevu wa mapato kwa taifa kama ilivyokuwa kwenye madini mengine. “Nafahamu kwamba Mauzo ya ubadilishano wa umiliki wa uchimbaji wa madini hayo yamefanyika kwa bei ya dola 1.16 ambayo ni zaidi ya trilioni 2 lakini ni vyema Wizara ikatupa majibu ya hatua ambazo zimefikiwa mpaka sasa,” alisema. Mnyika alibainisha kwamba iwapo Taifa lingepata asilimia 30 ya mauzo hayo kama kodi, taifa lingepata Sh600 bilioni ambazo ni fedha nyingi kuliko bajeti nzima ya Wizara ya Nishati na Madini kwa mwaka. Alisema ni vyema sasa serikali ichukue hatua za kudhibiti ukwepaji wa ulipaji kodi kwani jambo hilo litawezesha kuongeza mapato ya serikali katika mwaka wa fedha 2011/2012 kwa Wizara ya Nishati na Madini. Aidha Mnyika alisema ni wakati wa serikali sasa kutunga Sheria ya kuhakikisha kwamba mikopo kwenye makampuni ya uwekezaji wa madini katika mahesabu ya kodi isizidi asilimia 70 ya mtaji pamoja na kutunga Sheria kuhakikisha kwamba riba ya mikopo kwenye makampuni yanayohusiana haitaondolewa kwenye mahesabu ya kodi. “Kufanya marekebisho ya sheria kuhakikishe kwamba kodi ya mtaji inatozwa katika mauziano ya makampuni yote ya madini ambayo mali zake au uwekezaji wake uko nchini hata kama mauziano hayo yamefanyika nje ya nchi hii itawezesha kuliongezea taifa mapato. |
0 Comments