Pinda ataka mapendekezo ya kuboresha elimu nchini  


WAZIRI Mkuu , Mizengo Pinda amewataka wadau wa elimu nchini kutoa  mapendekezo halisi ya nini kifanyike katika kuboresha Sekta ya elimu nchini ambayo inaonekana kushuka.

Akizungumza Jijini Dar es Salaam jana,  katika ufunguzi wa semina ya siku tatu ya  wadau wa elimu iliyoandaliwa na Chuo Kikuu cha Dar es Salaam katikakitengo cha Shule ya Elimu yenye lengo la kujadili maendeleo ya elimu nchini, Pinda alisisitiza kupatiwa ufumbuzi wa tatizo hilo.

Pinda alisema kumekuwapo na changamoto mbalimbali zinazoikabili sekta ya elimu na kusababisha kutokusonga mbele kama inavyotakiwa , lakini mkutano huo utawezesha kujua suluhisho.

“Hapa mmekutanisha wadau mbalimbali  wa elimu , hivyo nawaomba kuja na mapendekezo stahiki ya nini kifanyike ambapo serikali itatumia mapendekezo yenu kuyafanyia kazi” alisema Pinda

Pinda alisema , Serikali kwa kutambua uwapo wa vifaa vya kufundishia kutoendana na malengo  katika shule za msingi na sekondari imeanza mkakati wa kuweka  uwiano sawa wa majengo na vifaa.

“Serikali inahakikisha inaweka uwiano kati ya vifaa na wanafunzi mfano uwapo wa madawati, walimu, maabara, vitabu, nyumba za walimu, hosteli, vyoo na vitendea kazi vingine vya kutosha” alisema Pinda na kuongeza:

Serikali  inaangalia upya sera ya elimu ili kuweza kuona ni jinsi gani tutaweza kuziboresha na kuendana na wakati huu wa sayansi na teknolojia.

Pinda alisema, upanuzi wa shule za msingi na sekondari vinakwenda sambamba na ukuaji wa shule za awali ambapo mbali na hivyo wanafunzi wanaojiunga na vyuo vya Ualimu wameongezeka.

“Uandikishaji wa Vyuo vya Ualimu umeongezeka kutoka 23,403 mwaka 2007 hadi kufikia 37,698 mwaka jana na elimu ya juu kutoka 45,501 mwaka 2006/2007 hadi kufikia 139,639”alisema Pinda

Aidha Pinda alisema Upanuzi wa sekta ya elimu imekuwa ikipewa kipaumbele katika  bajeti ya nchini kwani kila  mwaka tangu mwaka 2005/6 na mwaka  2010/2011 ukilinganisha na sekta zingine na kufikia asilimia 18 ya bajeti yote nchini.

Waziri Mkuu alisema , uwiano unaonesha mwalimu mmoja anafundisha wanafunzi 48 kwa mwaka 2011 ukilinganisha na anavyotakiwa kufundisha wanafunzi 40.

“Serikali imekuwa ikiongeza juhudi katika kupunguza pengo kwa kuanzisha  bajeti ya elimu, kuajiri walimu zaidi, kujenga maabara na kununua vitabu zaidi” alisema Pinda.

Mkuu wa Shule ya Elimu wa UDSM, Profesa Eustella Bhalalusesa alisema baada ya kuwapo kwa maneno mengi mitaani yanayoongelewa juu ya kuyumba kwa sekta ya elimu bila majibu wameandaa mkutano huo utakaokuja na suluhisho la nini kifanyike.

“Watu wanaongea bila ya kusema nini kifanyike katika kuboresha elimu nchini ndio maana kama kitengo cha elimu tumewakutanisha wadau mbalimbali watakao jadili matatizo yote na baada ya hapo tutakuja na mapendekezo” alisema Profesa
Bhalalusesa na kuongeza

Wanafunzi wanafeli mitihani,mitihani inavuja na hakuna anayesema nini sababu na wala kifanyike kipi lakini baada ya hapa kila kitu kitaanza kwenda sawa.

Naibu waziri wa Elimu na Mafunzo ya Ufundi Stadi,  Philipo Mulugo alisema baada ya fedha za rada kurejeshwa nchini , Sh85 bilioni zimetengwa kusaidia sekta ya elimu. “Wataalamu wetu wapo na nafanya mahesabu ili kuweza kujua ni kiasi gani cha fedha kati ya Sh85 bilioni ziingie katika elimu na kuzifanyia nini” alisema Mulugo.

Mulugo alisema fedha hizo kwa sehumu kubwa zitaelekezwa kununua vitabu na madawati katika shule za msingi ambazo ndizo zinakabiliwa na upungufu wa vitendea kazi hivyo.