Bakwata Yatangaza Sikukuu ya EID September Mosi
Mufti wa Tanzania Sheikh Abubakar Bin Zubeir amesema Septemba Mosi itakuwa ni Sikukuu ya Eid El-Adhaa baada ya mwezi Dhil-Hijjah (mfungo tatu) kuandama Magharibi ya Agosti 22 mwaka huu.

Mufti ameeleza hayo katika mkutano na  wanahabari leo Alhamisi  Agosti 24 katika hotuba yake iliyosomwa na msemaji wake Sheikh Khamis Mataka.

Mkutano huo umefanyika katika makao makuu ya Baraza la  Kuu la Waislam  Tanzania (Bakwata), Kinondoni ambapo Mufti Zubeir amesema baada ya mwezi huo kuandama na Agosti 23 mwaka huu ilikuwa ni sawa na Mwezi Mosi Mfungo Tatu  (Dhul-Hijjah)1438 Hijiriyyah.

"Napenda kuutangazia umma kuwa nimethibitisha mwandamo wa mwezi  na kwamba siku ya Agosti 31 ni siku ya kufunga Sunna ya Araf.Wakati Septemba Mosi ni sikukuu,"amesema Mufti Zubeir kupitia msemaji wake huyo.

Amesema maadhimisho ya sikukuu hiyo kitaifa yatafanyika Dar es Salaam na swala itafanyika katika uwanja wa Garden, nyumba ya Msikiti wa Taqwa uliopo Ilala Bungoni huku Baraza la Eid likifanyikia katika eneo hilo pia.

Kupitia sikukuu hiyo, Mufti Zubeir amewahimiza Waislamu kuzidisha ibada na kufanya kheri katika siku 10 tukufu za mfungo tatu na kuichukua vyema falsafa  ya Hijja katika kudumisha umoja ja mshikamano miongoni mwao.

"Waislamu watumie kipindi hiki cha mwisho  wa mwaka wa Kiislamu kutafakari na kumchamungu na kuimarisha maadili mema ndani ya jamii itakayokuwa bora na ya kupendana,"amesema Mufti Zubeir.