Mkurugenzi Mtendaji wa mgodi wa dhahabu wa Bulyanhulu Gold Mine Bw. Peter Burger ( wa kwanza kushoto) akizungumza na jopo la majajaji na sekretarieti iliyotembelea mgodi huo kwa ajili ya kumtafuta mshindi wa Tuzo ya Rais ya Huduma za Jamii na Uwezeshaji
Na Greyson Mwase, Kahama
Imeelezwa kuwa mgodi wa dhahabu wa Buzwagi umetumia zaidi ya shilingi bilioni 3.7 kwa ajili ya ujenzi wa barabara zenye urefu wa kilomita tano kwa kiwango cha lami katika mji wa Kahama mkoani Shinyanga.Hayo yamesemwa na meneja mahusiano wa kampuni hiyo Bi Dorothy Bikurakule mbele ya timu ya majaji kwa ajili ya kumtafuta mshindi wa tuzo ya Rais ya Huduma za Jamii na Uwezeshaji ambayo inaendelea na zoezi hilo katika mkoa huo.Bi Bikurakule alisema kuwa mara baada ya uongozi wa mgodi huo kufanya mazungumzo na mkuu wa wilaya pamoja viongozi wa halmashauri, ilikubaliwa barabara kujengwa katika kiwango cha lami katika mji wa Kahama ili kuchochea ukuaji wa uchumi wa mji huo.“Barabara ilikuwa ni moja ya vipaumbele muhimu vilivyowasilishwa katika mkutano mkuu wa viongozi wa halmashauri na mkuu wa wilaya, hivyo kama mgodi na viongozi tulikubaliana na kuanza kujenga barabara mara moja” alisema
Akielezea miradi mingine iliyotekelezwa na mgodi wa Buzwagi Bi Bikurakule alieleza kuwa ni pamoja na ufadhili wa masomo kwa wanafunzi 234 wanaosoma elimu ya sekondari katika shule mbalimbali zilizopo katika wilaya hiyo ambapo gharama yake ilikuwa ni shilingi milioni 39.4
Alisema lengo la ufadhili huo lilikuwa ni kuwawezesha wanafunzi wanaotoka katika familia zenye kipato cha chini kupata msingi wa elimu bora itakayopelekea kuwa wataalamu wa sayansi na kufanya kazi katika migodi ya madini.
Akielezea mikakati iliyofanywa katika kuhakikisha kuwa wananchi wananufaika na uwepo wa mgodi huo, Bi Bikurakule alisema kuwa mgodi uliwezesha vijana kuunda vikundi vidogo vidogo na kuwapatia elimu pamoja na vifaa kwa ajili ya kufyatua matofali mradi ambao tayari umeanza kutekelezwa.
Aidha, alisisitiza kuwa mgodi umekuwa ukitoa elimu na kuwezesha wananchi kuanzisha kampuni kwa ajili ya kutoa huduma katika mgodi huo ingawa kumekuwepo na changamoto ya kutotoa huduma kwa wakati au chini ya kiwango kinachohitajiwa na mgodi.
Akielezea mikakati iliyofanywa na mgodi katika kukabiliana na changamoto hizo Bi. Bikurakule alisema mgodi uliandaa mkutano wa wasambazaji wa ndani ya nchi ambapo elimu ya ujasiriliamali, sera na fursa ilitolewa.
Aliongeza kuwa katika kipindi cha Februari hadi Agosti 2014, wasambazaji wa ndani wapya 7 walisajiliwa na kusisitiza kuwa lengo ni kufikisha wasambazaji 10 mapema Desemba mwaka huu.
Wakati huo huo akizungumza na timu ya majaji Mkuu wa Wilaya ya Kahama Bw. Benson Mpesya alisema kuwa mgodi wa Buzwagi umekuwa chachu kubwa ya ukuaji wa uchumi wa mji wa Kahama hususani katika kutengeneza fursa kwa vijana wa kitanzania.
Aliongeza kuwa awali hali ya usalama haikuwa nzuri mgodini hapo lakini baada ya mgodi kuanza kuajiri wanavijiji wanaozunguka katika mgodi huo kama walinzi hali ya usalama mgodi hapo imeimarika
Alisisitiza kuwa mgodi hutumia shiligi milioni 53 kwa ajili ya kulipa wananchi wanaolinda mgodi huo na kusisitiza kuwa fursa zinazohitaji wataalamu zichangamkiwe na vijana ili kuchangia katika maendeleo ya nchi.
0 Comments