Mkurugenzi wa Utawala na Udhibiti wa SportPesa, Tarimba Abbas akizungumza jambo akiwa ameambana na Mkurugenzi Mkuu SportPesa Pavel Slavkov pamoja na Mkurugeni wa utawala wa Sportpesa Luca Neghesti.
Timu ya Simba leo imekabidhiwa kitita cha Sh. milioni 100 kutoka kampuni ya SportPesa Ltd ikiwa moja ya fedha walizoahidiwa na kampuni hiyo wakichukua Ubingwa wa Ligi Kuu Bara kwa mujibu wamkataba walioingia nayo kama wadhamini wao wakuu.Hafla ya makabidhiano ya kitita hicho imefanyika kwenye ofisi za SportPesa zilizopo maeneo ya Masaki jijini Dar es Salaam huku ikihudhuriwa na viongozi wa pande zote mbili sambamba na wachezaji wa Simba wakiongozwa na nahodha wao John Bocco ambaye alifanya zoezi la kukabidhi kombe kwa wadhamini hao.
Akizungumza kwenye hafla hiyo Kaimu Makamu wa Rais wa Simba, Iddi Kajuna, alisema kuwa: “Tunaishukuru sana SportPesa kwa kututia nguvu tangu mwanzo wa Ligi hadi leo hii ambapo wametukabidhi hundi hiyo ya shilingi milioni 100, bila kujali hata kuwa bado tuna mchezo mmoja ili tukamilishe ratiba yetu.
Afisa Mtendaji Mkuu wa SportPesa, Pavel Slavkov Akipokea Kombe la Ubingwa wa Ligi kuu Soka Tanzania kutoka kwa Nahodha wa Simba John Bocco (kulia) akimkabidhi kombe la ubingwa huku viongozi wengine kutoka Simba na kampuni hiyo wakishuhudia.
“Pia tunawashukuru SportPesa kwa kutuwezesha kulipa mishahara ya wachezaji wetu mapema, jambo ambalo tunaamini kwa namna moja au nyingine limechangia kwa kiasi kikubwa kwetu kuibuka mabingwa wa Tanzania kwani bila kutoa mishahara kwa wakati yawezekana leo hii tusingeweza kufikia malengo yetu alisema Kajuna.
Naye Mkurugenzi wa Utawala na Udhibiti wa SportPesa, Tarimba Abbas alisema: “Kwa niaba ya kampuni yetu ya SportPesa nawapongeza sana Simba kwa kuwatendea haki mashabiki wa Simba kwani kufanya hivyo mmetupa heshima kubwa sana sisi wadhamini wenu wakuu, kwani mmeitendea haki sana nembo yetu kiasi cha kampuni yetu kuamini kuwa imefanya jambo muhimu kuwa wadhamini wenu wakuu,” alisema Abbas.
0 Comments