Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano Profesa Makame Mbarawa amemtaka Mkandarasi Yapi Merkezi na Motaengil Africa anayejenga Reli ya kati ya kisasa (Standard Gauge) sehemu ya Dar es Salaam hadi Morogoro kilomita 205 kuhakikisha ujenzi huo unakamilika ndani ya miezi thelathini iliyopangwa.

Akizungumza mara baada ya kukagua tuta litakapojengwa reli hiyo kutoka pugu, soga hadi ngerengere profesa mbarawa amepongeza kazi inayoendelea na kumtaka mkandarasi kuongeza kasi ili kazi ya kutandika reli ianze katika muda mfupi ujao.

“Hakikisheni kazi ya ujenzi wa tuta na kiwanda cha kutengeneza mataruma ya zege vinakamilika katika muda wa miezi mitatu kutoka sasa ili kwenda na ratiba ya ujenzi huo,” amesema Profesa Mbarawa.

Profesa Mbarawa amekagua kiwanda cha kutengeneza mataruma ya zege yatakayotumika katika ujenzi wa reli hiyo na kusisitiza umuhimu wa mkandarasi kutoa fursa za ajira kwa wananchi wanaozunguka reli hiyo.

“Wale mtakaopata ajira katika reli hii hakikisheni mnafanyakazi kwa bidii na uaminifu ili kuwezesha ukenzi kuwa katika ubora unaotakiwa na kukamilika kwa wakati”, amesisitiza profesa Mbarawa.
Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano Profesa Makame Mbarawa akikagua ujenzi wa tuta kwa ajili ya njia ya reli alipotembelea eneo la Soga (Kibaha) wakati wa ziara yake ya kukagua maendeleo ya ujenzi wa Reli ya kiwango cha kimataifa (Standard Gauge) yenye urefu wa kilomita 205 kutoka Dar – Morogoro leo. Kutoka kulia ni Meneja Mradi wa SGR Mhandisi Maizo Mgedzi, Meneja wa Kanda ya Afrika Mashariki wa Kampuni ya Yapi Merkezi Bw. Abdullah Kilic na Mhandisi Felix Nnalio.
Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano Profesa Makame Mbarawa akifafanua jambo mbele ya Meneja wa Kanda ya Afrika Mashariki wa Kampuni ya Yapi Merkezi Bw. Abdullah Kilic (katikati) alipofanya ziara ya kukagua maendeleo ya ujenzi wa Reli ya kiwango cha kimataifa (Standard Gauge) ambapo awamu ya kwanza inajengwa kutoka Dar – Moro yenye urefu wa 205km.
Muuonekano wa awali wa tuta la reli linaloendelea kujengwa kwa kuondolewa tabaka la udongo wa kilimo na kuwekewa udongo wa ujenzi katika eneo la Soga (Kibaha) ambapo mradi wa ujenzi wa reli ya kisasa unaendeleo.
Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano Profesa Makame Mbarawa akitazama kifaa cha kupima mgandamizo wa ardhi mara baada ya ardhi kushindiliwa alipokagua ujenzi wa tuta la reli katika eneo la Soga (Kibaha).
Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano Profesa Makame Mbarawa akiendelea na shughuli ya ujenzi wa karakana ya kutengeneza mataluma ya reli alipokagua ujenzi alipofanya ziara katika eneo la Soga (Kibaha).