Aliyekuwa kada wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) ambaye katika Uchaguzi Mkuu wa 2015 alichukua fomu ya kugombea Ubunge wa Jimbo la Kawe, Dar, lakini kura za maoni hazikutosha, Kolman Vincent Massawe amefariki dunia kwa ajali mbaya ya gari iliyotokea kwenye Barabara Kuu ya Bagamoyo eneo la Msata mkoani Pwani.
Kwa mujibu wa mashuhuda, ajali hiyo ilitokea usiku wa kuamkia Jumatano, wiki hii maeneo hayo ambapo ajali hiyo ilihusisha fuso na gari ndogo alikuwa akiendesha Kolman ambapo ndani yake alikuwa peke yake. Akithibitisha kutokea kwa ajali hiyo jijini Dar, leo, Kaimu Katibu Mkuu wa Umoja wa Vijana wa CCM (UVCCM-MNEC), Shaka Hamdu Shaka amesema:
“Sikuamini hadi leo (wakati wa kuaga) kumuona na kumuaga kwa macho ndugu yetu, rafiki yetu, kada wetu, mpiganaji mwenzetu wa mstari wa mbele, Kolman Vincent Masawe ambaye ameitwa na Mwenyezi Mungu na ameitika, kazi ya Mungu haina makosa. Mbele yake, nyuma yetu.”
Kolman ni mtoto wa Vincent Massawe ambapo baba yake huyo anatajwa kumiliki Kampuni ya Ujenzi ya Skol Building Contraction ambaye ni miongoni mwa makampuni ya ujenzi ambayo hivi karibuni Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda alizisimamisha kupewa tenda hadi atakapojiridhisha juu ya utendaji wake wa kazi.
Kwenye uchaguzi huo wa mwaka 2015, Kolman alizidiwa kura za maoni ili kugombea katika Jimbo la Kawe ambapo aliangushwa na Kippi Warioba. Kolman ameagwa leo nyumbani kwake, Masaki jijini Dar na mwili wake kusafirishwa kwenda mkoani Kilimanjaro kwa mazishi.
0 Comments