Kampuni ya Lugumi Enterprises Ltd iliyotajwa katika sakata la zabuni ya Sh34 bilioni ya kuweka mashine za kielektroniki za kuchukua alama za vidole ya Jeshi la Polisi, iko hatarini kupoteza mali zake kutokana na kudaiwa kodi na Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA).
Mnada wa maghorofa hayo utafanywa na kampuni ya udalali ya Yono Auction Mart, kwa niaba ya TRA Mkoa wa Ilala. Maghorofa hayo yapo maeneo tofauti jijini Dar es Salaam; moja Mtaa wa Mazengo, Upanga na mawili yako Mbweni JKT wilayani Kinondoni.
Kuuzwa kwa maghorofa hayo kumetangazwa jana katika gazeti la Serikali la Sunday News, tangazo hilo likieleza kwamba ghorofa la Upanga linafaa kwa ofisi wakati yale ya Mbweni JKT yanafaa kwa makazi.
Mkurugenzi mtendaji wa Yono, Scolastica Kevela alisema mnada huo utafanyika Septemba 9, kuanzia saa 4:30 asubuhi kwenye maeneo yalipo maghorofa hayo. Kevela alisema Lugumi Enterprises imeshindwa kulipa kodi ya TRA kwa wakati ndiyo maana wakapewa kazi ya kuuza majengo hayo.
Mkurugenzi huyo alikataa kutaja kiasi ambacho Lugumi anadaiwa na TRA pamoja na thamani ya maghorofa hayo. Kevela alitoa rai kwa Watanzania kujenga utamaduni wa kulipa kodi kwa wakati ili kuepuka usumbufu unaoweza kujitokeza.
Kwa mujibu wa tangazo hilo, masharti ya mnada ni kulipa asilimia 25 ya thamani ya bei kwa atakayefanikiwa kuyanunua maghorofa hayo. Kiasi kilichobaki kitatakiwa kulipwa ndani ya siku 14, tangu siku ya mnada na kwamba atakayeshindwa kulipa katika kipindi hicho hatarudishiwa fedha alizotoa na mnada utafanyika kwa mara nyingine. Ukaguzi wa nyumba hizo unatakiwa kufanywa siku 10 kabla ya siku ya mnada.
Akizungumzia hilo, mkurugenzi wa huduma na elimu ya mlipakodi wa TRA, Richard Kayombo alisema Lugumi inadaiwa kodi za aina mbalimbali zinazotokana na mapato yake.
Lugumi ilikuwa gumzo mwaka jana baada ya taarifa ya CAG kuonyesha kuwa ililipwa zaidi ya ssilimia 90 ya fedha za zabuni kwa ajili ya kuweka vifaa hivyo katika vituo 138, lakini hadi wakati wa ukaguzi ilikuwa imeweka katika vituo 14 tu. Taarifa hiyo ilifika bungeni na kuundwa kamati ndogo ambayo ilichunguza na kuwasilisha taarifa.
0 Comments