MKUU wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda, leo ametoa msaada wa gari aina ya Noah, pikipiki tatu, kompyuta tano na Camera mbili za kisasa kwa Shirika la Utangazaji Tanzania (TBC) ili kuongeza nguvu katika kuwafikia wananchi.
Mbali na vifaa hivyo vya kisasa,  Makonda amefanikiwa kumpata mfadhili atakayepaka rangi jengo lote la TBC kuanzia  kesho ili liwe na mwonekano wa kisasa.
Toyo zilizokabidhiwa na mkuu wa mkoa.
Akizungumza baada ya kukabidhi msaada huo, Makonda amesema lengo ni kuwawezesha wananchi ambao hawana uwezo wa kuita vyombo vya habari na kueleza matatizo yao, waweze kufikiwa.
Mkuu huyo wa mkoa ametoa msaada huo baada ya kufika hapo na kubaini uwepo kwa changamoto za vifaa ikiwa pamoja na usafiri na vitendea kazi vingine vinavyowafanya wafanyakazi na wahariri kushindwa kutekeleza majukumu yao kikamilifu.
Noa zilizokabidhiwa na Makonda.
Vifaa hivyo vitatumika kuongeza nguvu kwenye kipindi cha Hadubini ambacho kimekuwa kikiwasaidia wananchi wanyonge kupaza sauti zao.
Naye Kaimu Mkurugenzi wa TBC, Martha Swai, amemshukuru kiongozi huyo wa mkoa kwa kuwapatia msaada huo ambapo pia mtayarishaji wa kipindi cha Hadubini, Zaituni Mkwama, alieleza kuwa vifaa hivyo vitawaongezea ufanisi katika kazi yao.