Baada ya Rapa Roma Mkatoliki kuachia ngoma ya Zimbawe inayozungumzia matukio ya kutekwa, msanii Moni Centrozone amefunguka na kumlalamikia Roma kuzunguzia tukio hilo pasipo kumuhusiasha mtu yoyote kwenye wimbo na kudai amejichukulia kama kinara mkuu.
Moni amedai kuwa anamshangaa msanii huyo kujizungumzia yeye binafsi kwenye ngoma ya Zimbabwe wakati tukio hilo liliwakuta wote na pia walikubaliana kutozungumza jambo lolote lile kuhusiana na yale yaliyowatokea lakini Roma yeye akaamua kufanya ndivyo sivyo.
"Kajiongelea yeye mwenyewe katika wimbo, kazungumzia nafsi ya kwanza umoja. Alisema atakaa kimya hataki kuzungumzia tukio la utekwaji lakini kaja katoa 'ngoma' ambayo inazungumzia mambo kibao kuhusu kilichotutokea. Itakuwa haina maana yeye kuni-mind mimi nikitaka kuzungumzia yaliyotukuta kipindi kile", alisema Moni.
Pamoja na hayo, Moni aliendelea kwa kusema "Nikipata 'vibe' naweza kuamua na mimi nikatoa dude lolote ambalo litanizungumzia mimi peke yangu na maisha yangu jinsi nilivyotekwa, kwa sababu kuna matukio ambayo na mimi nayakumbuka kipindi napatiwa mateso kwa sababu ngoma iliyotoka haikuniwakilisha mimi. Roma kajizungumzia mwenyewe kama ndiyo muhusika mkuu, huwezi kujua na mimi naweza kuwa nimeshaandaa mipango yangu ya kuzungumza kwani njia zipo nyingi". 
Hata hivyo Moni amesema haijalishi ni muda gani atachukua na yeye kusema chochote kuhusiana na kilichowahi kumtokea wakati akiwa ametekwa baada ya Roma kuachia ngoma ya Zimbabwe.
"Haijalishi kama nitaandaa 'press' kuelezea umma kilichotukuta au nitaanda wimbo wangu kuzungumzia na mimi kilichonikuta, kwa sababu haya ni maisha yangu na mimi sijazaliwa na mtu nimezaliwa peke yangu", alisisitiza Moni.