Shose Mori Sinare akiwa mahabusu.
Mrembo Shose Sinare, ambaye alitwaa taji la Miss Tanzania mwaka 1996, ameweka rekodi inayoweza kuwa ngumu kuvunjwa, baada ya kukaa gerezani kwa siku 503 hadi kufikia leo, akikabiliwa na makosa kadhaa, likiwemo la kutakatisha fedha ambalo kwa mujibu wa sheria za nchi, halina dhamana.
Shose, ambaye ushindi wake kwenye mashindano ya mwaka huo ulipokewa kwa matumaini makubwa ya kufanya vizuri katika taji la dunia, alipandishwa kizimbani kwa mara ya kwanza Aprili Mosi, 2016 na tangu wakati huo, hakuwahi kuonja upepo wa uraiani.

Shose Mori Sinare (kulia) akiwa kortini.

Wema Sepetu, aliyetwaa taji la Miss Tanzania miaka 10 baada ya Shose, ni mrembo mwingine ambaye amekutana na mkono wa sheria mara kadhaa kwa makosa tofauti, lakini linalomtesa hivi sasa ni lile la kudaiwa kukutwa na madawa ya kulevya aina ya bangi nyumbani kwake Februari 3, mwaka huu.
Wema alikaa mahabusu kwa zaidi ya wiki moja kabla ya kupandishwa kizimbani katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, akishtakiwa kwa kosa hilo la kukutwa na bangi pamoja na karatasi zake za kusokotea.


Shose Mori Sinare.
Ingawa kumekuwa na wasichana wengine waliowahi kutwaa taji hilo ambao wamekutana na kadhia ya kukabiliwa na vyombo vya sheria, ikiwemo ya kuwekwa lupango kwa makosa mbalimbali, ofisa huyu wa zamani wa benki ya Stanbic amewazidi kwa mbali.
Mrembo mwingine ambaye aliwahi kupatwa na misukosuko na vyombo vya sheria ni Miss Tanzania 2009, Miriam Gerald, ambaye alijikuta akimaliza siku tatu akiwa mahabusu, baada ya kukamatwa kwa kosa la kuvunja kioo cha gari la muigizaji mmoja maarufu nchini.

Wema Sepetu.
Shose Mori Sinare ambaye alikuwa Mkuu wa Idara ya Ushirikiano na Uwekezaji wa Benki ya Stanbic Tanzania, alipandishwa kizimbani pamoja na aliyewahi kuwa Kamishna Mkuu wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), Harry Kitilya na Sioi Solomon, aliyekuwa Mwanasheria Mkuu wa Benki ya Stanbic Tanzania.
Wote watatu wanashtakiwa kwa makosa ya kula njama za udanganyifu, kugushi nyaraka na kutakatisha fedha, tuhuma ambazo zimewafanya kusota mahabusu kwa muda wote huo wa zaidi ya mwaka mmoja na nusu.