Marais wastaafu, Benjamin Mkapa na Jakaya Kikwete wamekutana kwa mara ya kwanza katika jukwaa moja wakiwa nje ya nchi wakihudhuria mkutano unaoratibiwa na Uongozi Institute kwa kushirikiana na Taasisi ya Mbeki.Mkutano huo unaomalizika leo unafanyika Johannesburg Afrika Kusini na kuhudhuriwa na marais kadhaa wastaafu.Hii ni mara ya kwanza kwa marais hao kushiriki tukio la pamoja wakiwa nje ya nchi tangu Rais Kikwete aondoke marakani mwaka 2015. Ingawa viongozi hao wamekuwa wakishiriki katika shughuli mbalimbali za kimataifa lakini hawajawahi kukaa jukwaa moja wakiwa nje ya nchi.Marais wengine wastaafu wanaohudhuria mkutano huo ni pamoja na aliyekuwa Rais wa Nigeria, Olusegun Obasanjo na Hassan Sheikh Mohamud aliyekuwa rais wa Somalia.
Picha za video zinazorusha mkutano huo zimewaonyesha marais hao wakiwa katika jukwaa moja wakipiga picha baada ya kumaliza majadiliano ya sehemu ya kwanza.
Katika upigaji picha, Rais Kikwete ameonekana akiwa ameketi mwanzo akiwafuatiwa na rais wa Nigeria, Obasanjo na kisha kufuatiwa na Mahamud wa Somalia. Rais Mkapa ameketi nafasi ya nne akifuatiwa na kiongozi mwingine ambaye hakuweza kutambulika mara moja na mwishoni aliketi Rais Thabo Mbeki ambaye taasisi yake ndiyo mwenyeji wa mkutano huo.
Mara baada ya kumalizika kwa shughuli ya upigaji picha, Rais Kikwete alionekana akijadiliana jambo kwa karibu na Rais Obasanjo na kisha viongozi hao waliteremka kutoka jukwaani.
Wakati akielekea kwenye eneo lake Kikwete aliwasalimia wageni kadhaa ndani ya mkutano huo na baadaye alielekea sehemu aliyokuwa amesimama aliyekuwa katibu mkuu kiongozi, Ombeni Sefue na kuonekana akimsisitizia jambo na kisha akaondoka.
Viongozi hao wamekuwa wakijadiliana kuhusu masuala ya demokrasia, utawala bora na jinsi ya kuzisaidia nchi za Afrika kusonga mbele kimaendeleo.
0 Comments