Jidenna Theodore Mobisson.I’M a classic man, you can be mean when you look this clean, I’m a classic man…” (Mimi ni mwanaume wa kiwango cha juu, utakuwa na maana kama ukiwa msafi kama hivi…) hicho ni kibwagizo cha wimbo wa Classic Man, uliomtambulisha Jidenna Theodore Mobisson katika ulimwengu wa muziki wa Hip Hop, mwanzoni mwa mwaka 2015.
Kabla ya hapo, hakuna aliyekuwa anamjua Jidenna na baada ya kuachia ngoma yake hiyo ya kwanza, alifanikiwa kutinga kwenye nafasi ya 49 kwenye chati kubwa ya muziki ya Billboard na kumpatia tuzo ya mwanamuziki bora anayechipukia ya Soul Train Music Awards nchini Marekani.
Aliteuliwa pia kuwania tuzo ya msanii bora chipukizi kwenye Grammy Awards ingawa hakushinda, baadaye mwaka huu, 2017 akaachia ngoma nyingine ambayo inakimbiza sana kwa sasa, Bambi (My Dear). Baada ya kuachia Classic Man, Jidenna alianza ku-make headlines, hasa kutokana na utanashati wa hali ya juu aliouonesha kwenye video ya wimbo huo na kilichokuja kuwashangaza wengi, ni pale mwenyewe alipofunguka kwamba chimbuko lake ni nchini Nigeria.
Licha ya kueleza kwamba asili yake ni Nigeria, kuna kitu kilionekana kutokuwa sawa kwa Jidenna kwani mara kwa mara alikuwa akiizungumzia vibaya nchi yake kwenye mitandao ya kijamii, akitoa matamshi ambayo yalionesha kuwakera sana mashabiki wake wa nchini Nigeria, na hapo ndipo alipoamua kumwaga nyongo.
Katika mahojiano na VLAD TV, Jidenna ambaye baba yake, Oliver Mobisson alikuwa Mnigeria mweusi kutoka kabila la Igbo, akiwa ni Profesa wa Sayansi ya Kompyuta katika Chuo Kikuu cha Enugu, Nigeria, na mama yake, Tama Mobisson akiwa ni Mmarekani mweupe, alifunguka kwamba kutokana na rangi ya ngozi yake (chotara wa Kizungu na Kinigeria), amewahi kupigwa risasi ya mguu akiwa na umri wa miaka mitano.
Si kupigwa risasi tu bali pia mama yake alipigwa vibaya mbele ya macho yake na baba yake akaporwa kiwango kikubwa cha fedha na majambazi, kipindi hicho wakiwa wanaishi nchini Nigeria. Shambulio hilo, lilisababisha baba yake kuamua kuhamishia makazi yake nchini Marekani, katika Mji wa Norwood, Massachusetts kwa ajili ya usalama wa familia yake na huko ndiko alikokulia na baadaye alipoanza kujitegemea, alihamia Brooklyn, New York anakoishi hadi leo.
Jidenna Theodore Mobisson.
“Rangi yangu nyeupe, na asili ya Kizungu ya mama yangu, vilisababisha tunusurike kuuawa. Ukiwa mweupe Nigeria, unaonekana una fedha, na kwa sababu watu wengi ni maskini, unakuwa kwenye hatari ya kuvamiwa, kutekwa na kuuawa muda wowote na majambazi na makundi ya kigaidi, hicho ndicho kilichotokea kwangu,” alikaririwa Jidenna.
Akaendelea kufunguka kwamba, hata baada ya baba yake mzazi kufariki nchini Marekani kwa ugonjwa wa shambulio la moyo, suala la kurudi kumzika nchini Nigeria, lilikuwa mtihani mkubwa kwa wanafamilia. “Kwa kuwa familia yetu wote ni weupe isipokuwa baba, wakati wa kwenda kumzika baba nyumbani, tulilazimika kukodi bunduki nyingi za AK-47 na makomando kwa ajili ya ulinzi wakati wote wa mazishi, walitulinda kuanzia mwanzo mpaka tulipomaliza na kurejea nchini Marekani,” alisema.
Jidenna mwenye umri wa miaka 31, anasema licha ya yote yaliyotokea, bado anajivunia asili yake ya Nigeria na mashabiki wake wanapaswa kumuelewa kwamba kuna muda huwa kumbukumbu za kuumiza zinamjia ndani ya kichwa chake na kusababisha atoe maneno makali kuhusu nchi hiyo.



Jidenna Theodore Mobisson.





Katika video ya Bambi iliyopo kwenye albamu yake ya kwanza ya The Chief, Jidenna amemtumia mwanadada wa Nigeria, Megalyn Echikunwoke ambaye amecheza nafasi ya mpenzi wake aliyeamua kumsaliti na kwenda kuolewa na mwanaume mwingine, tena mweusi, Jay Ellis ambaye pia ni Mnigeria.



“Sina kinyongo na Nigeria na ndiyo maana hata kwenye video zangu nawatumia Wanigeria,” alisema Jidenna ambaye utanashati wake kwenye video zake na maisha ya kila siku, umempa umaarufu mkubwa.

NA: HASHIMU AZIZ KWA MSAADA WA MITANDAO| UWAZI JUMANNE