TAARIFA zilizotufikia hivi punde zinaeleza kuwa, Mbunge wa Singida Mashariki (CHADEMA) na Rais wa Chama cha Mawakili Tanganyika (TLS), Tundu Lissu amekamatwa na Mlinzi wa amani alipokuwa anatoka mahakamani Kisutu huku ikielezwa kuwa wamemkamata kwa ajili ya mahojiano.
“Tumetoka Mahakama ya Kisutu muda huu ambapo Mwanasheria Mkuu wa Chama (CHADEMA), Tundu Lissu alikuwa na kesi ya tuhuma za uchochezi (uchochezi one) lakini pia alikuwa ni wakili kwenye kesi inayomkabili Yericko Nyerere hapahapa Kisutu.
“Wakati gari la Lissu likiwa getini tayari kwa kutoka, likazuiliwa. Nyuma ya gari yake pia likasimama gari jingine likiwa na askari polisi wenye silaha, kisha wengine wakamfuata na kumwambia yuko chini ya ulinzi na kutakiwa kwenda Kituo Kikuu cha Polisi (Central Police).
“Wakamtaka ashuke kwenye gari lake na apande gari jingine la kwao kwa ajili ya kuelekea Central Police,” amesema Msemaji wa Chadema, Tumaini Makene.