KWA mara nyingine, ninapenda kuchukua nafasi hii kumshukuru sana Mwenyezi Mungu, mwingi wa rehema kwa kuweza kunifikisha hapa leo, kiasi cha kuweza kuzungumza na nyinyi leo kupitia safu yetu hii.
Ninasema kila mara kwamba ukarimu wa Mwenyezi Mungu ni wa ajabu sana, kwa sababu anaweza kutenda miujiza hata kwa watu ambao hadi leo hawajaona umuhimu wake na wanafanya mambo kana kwamba wao ndiyo wenye ufalme hapa duniani. 
Hakuna mwenye uwezo wa kuzuia lolote ambalo Mungu atataka kulifanya juu yetu, anapokaa kimya wakati sisi tukifanya mambo yenye kumkwaza, hanyamazi kwa sababu tunaweza kumuepuka, la hasha, anakaa kimya kwa sababu ya huruma yake, anafahamu kwamba tunao uwezo wa kujirudi na kujirekebisha.

Nirudie tena kuwaomba kutafuta muda wa kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa sala.

Baada ya kusema maneno hayo, naomba sasa nirejee kwenye mada yetu ya leo ambayo inazungumzia juu ya wizi wa muda mrefu unaofanywa katika ofisi nyingi za serikali kwa kutumia majina ya watu wasiokuwepo kazini, waliofariki au ambao wamefukuzwa kazi. 

Mtindo huu wa wizi ni wa miaka nenda rudi, unafanywa kwa ushirikiano kati ya maofisa wa ofisi husika na Hazina, kwa ofisi zile ambazo watumishi wake wanalipwa moja kwa moja kupitia wizarani. Wafanyakazi wa Idara zingine ambao mishahara yao haipiti huko, nao wizi wao hufanywa kwa kuwahusisha wakubwa wao wakishirikiana na uhasibu. 

Mwishoni mwa wiki nilisoma mahojiano ambayo Naibu Waziri wa Fedha, Mwigulu Nchemba alifanya na chombo kimoja cha habari, akizungumzia jinsi ambavyo serikali inapoteza fedha nyingi kupitia wizi huu. Alisema kwamba kwa mwaka mmoja, serikali yetu inapoteza kiasi cha shilingi Trilioni 1.6 kwa watu kulipwa mishahara hewa. 

Kiasi hiki cha fedha ni kikubwa sana, ni bajeti ya Wizara nzima kwa mwaka. Lakini imekuwa ikipotea huku ikionekana kama vile ni jambo la kawaida, wakati tuna mahitaji mengi ya msingi ambayo yangeweza kutatuliwa kwa fedha hizi zinazopotea ovyo