Jalada la kesi namba MAG/RB/8329/2014- WIZI kwenye Kituo cha Polisi cha Magomeni, Dar, limefunguliwa na mwanaume aitwaye Rashidi akimshitaki mkewe, Fatuma Ally akimtuhumu kwa wizi wa mwanaye Zainabu Rashidi aliyemwandikisha jina la mwanaume mwingine aliyetajwa kwa jina la Paulo Mlela.
Rashidi alisema kwamba alipofika Muhimbili alishangaa alipojikuta akiwekwa chini ya ulinzi na kuhojiwa kwa muda na madaktari akidaiwa ni mwizi wa mtoto.Alisema, aliwaonyesha kadi ya kliniki ya mtoto Zainabu yenye jina lake (Rashidi) akiwa ndiye baba mzazi wa mtoto huyo, jambo ambalo madaktari hao walilishangaa.
Bw. Rashidi akiwa amembeba mwanaye, Zainabu Rashidi. Hata hivyo, madaktari hao walimwachia kwa sharti la kutopatiwa cheti cha kuzaliwa hadi ampeleke Paulo Mlela ambaye jina lake lipo kwenye makabrasha hospitalini hapo likionyesha naye ni baba mzazi wa Zainabu.
Katika kudadisi, Rashidi alionyeshwa fomu ya discharge (kuruhusiwa) baada ya mkewe kujifungua iliyoonyesha jina la Paulo Mlela kama mume wa Fatuma badala ya jina lake, jambo lililomchanganya na kuamua kufuatilia ukweli kwa mkewe ambaye alikataa tuhuma hizo na kudai kuwa hakuwa akijielewa wakati fomu hiyo ilipokuwa inajazwa kwa kuwa alikuwa ametoka kujifungua.
Rashidi alisema kuwa siku mkewe alipokuwa anajifungua yeye na ndugu zake wa karibu walikuwa safarini mazishini hivyo huenda mwanaume huyo alipata nafasi ya kuingiza jina lake. Rashidi alisema aliamua kumtafuta Paulo kisirisiri ndipo akagundua kuwa anaishi mtaa wa pili kutoka nyumbani kwake na mara kadhaa aliwahi kumwona akiwa na mkewe.
Akizungumzia hatua ambazo alizichukuwa, Rashidi alidai kuwa amelifikisha suala hilo polisi na baraza la kata ambako linashughulikiwa kupitia ustawi wa jamii.Rashidi aliongeza kwamba, kwa sasa mkewe ameondoka nyumbani.
0 Comments