Pia mume wa mtu ni sumu! Kikongwe wa miaka 70 aliyejitambulisha kwa jina la Gwerino Ganga amemtwanga risasi mbili mwanaume aitwaye Thadei Mbungu (40) akimtuhumu kuingilia ndoa yake kwa kuvunja amri ya sita na mama watoto wake.
Thadei Mbungu enzi wa uhai wake.Tukio hilo la ajabu lilijiri Oktoba 9, mwaka huu mkoani Iringa ambapo mashuhuda wanadai Mbugu, mbali na kukutwa na mke wa mtu siku hiyo, alimjibu mwenye mke majibu yenye kuumiza moyo mbele ya watu waliokuwa wakinywa pombe katika klabu cha pombe za kienyeji.Ilidaiwa kuwa, awali mtuhumiwa huyo wa mauaji alikuwa akimsaka marahemu ambaye alidai amekuwa akiivuruga ndoa yake.
Akizungumza na mwandishi wa habari hizi aliyefika eneo la tukio, mtoto wa kambo wa mtuhumiwa alisema chanzo cha mauaji hayo ni mke wa Mbungu kumtuhumu mama yake (mke wa mtuhumiwa) kuwa ana tabia ya kukopa fedha kwa mumewe (marehemu) hali iliyosababisha mama huyo kwenda kumwita baba yake (mtuhumiwa) na kumshitakia maneno hayo.
Kufuatia kauli hiyo, mtoto huyo wa mtuhumiwa alisema baba yake alimtaka marehemu na mkewe kuondoka klabuni hapo kwa vile wamependana na kwenda kuishi pamoja lakini marehemu aligoma na kuendelea kutoa lugha yenye kuudhi.
“Baada ya hapo mimi nilitoka kwenda kutafuta msaada wa watu kuja kuamua ugomvi huo kwa kumtoa marehemu, lakini ghafla nilisikia mlio wa risasi, nikarudi mbio na kukuta marehemu akitoka nje huku akivuja damu baada ya kupigwa risasi ya bega la kushoto,” alisema mtoto huyo.
Mke wa mtuhumiwa huyo, Melea Mtwanga alisema hajapata kuwa na uhusiano wa mapenzi na marehemu ila aliuawa kwa sababu ya lugha zake chafu.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Iringa, Ramadhan Mungi amethibitisha kutokea kwa tukio hilo na mtuhumiwa anashikiliwa huku akisema bunduki hiyo aina ya shot gun ilikuwa ikimilikiwa kihalali.
0 Comments