Mtu mmoja asiyefahamika jina wala makazi yake, umri kati ya miaka 25 – 30 amefariki dunia wakati akiwa anapatiwa matibabu baada ya gari lenye namba za usajili T.397 AQT aina ya Isuzu lililokuwa likiendeshwa na dereva aitwaye Noel Mahenge kugongana na gari lenye namba za usajili T.505 BYG/T.843 CUG aina ya Scania likiendeshwa na dereva aitwaye Godfrey Philimon (37) mkazi wa Tukuyu wilaya ya Rungwe.

Ajali hiyo imetokea jana majira ya saa 09:45 asubuhi huko Chapwa, kata na tarafa ya Tunduma, wilaya ya Momba, mkoa wa Mbeya katika barabara ya Mbeya/Tunduma. 
Aidha, katika ajali hiyo watu wawili walijeruhiwa na kulazwa katika hospitali ya serikali tunduma ambao ni 1. Shabani Kipande (22) mkazi wa Uyole na 2. Muddy Mselemu (25). Chanzo cha ajali ni mwendo kasi wa gari T.397 AQT aina ya Isuzu. Dereva alikimbia mara baada ya ajali na jitihada za kumtafuta zinaendelea. Mwili wa marehemu umehifadhiwa katika hospitali ya serikali Vwawa – Mbozi. 
Kamanda wa polisi mkoa wa Mbeya kamishina msaidizi mwandamizi wa polisi Ahmed Msangi anatoa wito kwa madereva kuwa makini wanapotumia vyombo vya moto ikiwa ni pamoja na kuzingatia sheria na alama za usalama barabarani ili kuepuka ajali zinazoweza kuepukika. Aidha, anatoa wito kwa yeyote mwenye taarifa za mahali alipo dereva aliyekimbia kuzitoa katika mamlaka husika ili akamatwe na hatua za kisheria zichukuliwe dhidi yake.