Mkuu wa mkoa wa Iringa Dkt Christine Ishengoma akizungumza na wanahabari jioni la leo ofisini kwake
Wanahabari Iringa wakimsikiliza mkuu wa mkoa wa Iringa
Mkuu wa mkoa wa Iringa akisikiliza maswali ya wanahabari waliofika kumsikiliza
Baadhi ya wanahabari mkoa wa Iringa wakitoka kumsikiliza mkuu wa mkoa leo
Mmiliki wa mtandao huu mzee wa matukio daima akiandaa kipindi kwa ajili ya kituo cha runginga cha Manispaa ya Iringa (IMTV) baada ya kutoka kwa mkuu wa mkoa mpiga picha ni Vicent Msigwa jembe
SERIKALI mkoa wa Iringa imepinga vikali taarifa za upotoshaji zilizotolewa na kituo kimoja cha TV hapa nchini kuhusu kuwepo kwa maandamano ya wakulima wa mpunga Pawaga ambao wanapinga ushuru wa mazao na kuwa habari hiyo haikuwa na ukweli kwani waliofanya maandamano hayo ni wafanyabiashara wa mpunga ambao walivaa kofia za wakulima ili kuendelea kuwanyosha wakulima.
Akizungumza na wanahabari leo ofisini kwake mkuu wa mkoa wa Iringa Dkt Christine Ishengoma alisema kuwa kituo hicho cha Runinga maarufu hapa nchini (jina tunalo) kilitangaza habari za kupotosha umma kuwa wakulima wa mpunga pawaga wameandamana hadi ofisi ya Halmashauri ya wilaya Iringa kupinga ushuru mkubwa wa mpunga jambo ambalo si kweli.
Alisema kuwa waliofanya maandamano hayo hawakuwa wakulima bali wakuliwa wafanyabiashara wa mpunga waliopo mjini Iringa kwa lengo la kuidanganya serikali kama ni wakulima wakati si kweli.
Kwani alisema kuwa lengo la wafanyabiashara hao ni kutaka kuendelea kuwanyonya wakulima na sio vinginevyo na hivyo kuwataka wanahabari kuwa makini katika kuandika habari na kuwa kabla ya kutangaza basi kufanya uchunguzi wa kina ili kuwa na usahihi badala ya kutoa habari za kupotosha umma.
Dkt Ishengoma alisema kutokana na maandamano hayo vyombo vya usalama mkoani hapa vimewahoji wafanyabiashara hao na kukubali kudanganya umma kuwa wao ni wakulima wa mpunga .
Hivyo alisema hatua ambazo zimechukuliwa kwa wafanyabiashara hao ni pamoja na kutakiwa kulipa ushuru na kuwa hatua nyingine za kisheria zitachukuliwa dhidi yao kwa tukio hilo.
Hata hivyo alisema kuwa hakuna mkulima ambae amekuwa akitozwa ushuru kwa zao lao la mpunga na kuwa ushuru uliopo ni kwa wafanyabiashara na si mkulima.
Pia mkuu huyo wa mkoa aliwataka wakulima mkoani hapa kuwa makini na mbinu chafu za wafanyabiashara katika uuzaji wa mazao yao ikiwa ni pamoja na kuzingatia vipimo halali katika kuuza mazao badala ya kuuza mazao yao kwa matakwa ya wanunuzi ya kutumia vipimo vya lumbesa ambavyo vimepigwa marufuku mkoani Iringa.
0 Comments