Mwalimu wa Taaluma wa
Shule ya Sekondari Maneromango iliyopo Kata ya Maneromango, Wilaya ya Kisarawe
mkoani Pwani, Jonas Buheruko akifanya mahojiano na Ripota wa Globu ya Jamii
(hayupo pichani) jana ofisini kwake.
Baadhi ya wanafunzi wa
kidato cha nne wa Shule ya Sekondari Maneromango iliyopo Kata ya Maneromango,
Wilaya ya Kisarawe mkoani Pwani wakifanya mitihani yao ya majaribio ya robo
muhula jana.
Na Joachim Mushi -
Kisarawe
WANAFUNZI 159 wa Shule
ya Sekondari Maneromango wametoroka kufanya mitihani ya majaribio ya robo
muhula iliyoanza juzi katika shule hiyo.
Wanafunzi hao ambao ni
vidato mbalimbali kuanzia cha kwanza hadi cha nne,ni kati ya wanafunzi 383 wa
Shule ya Sekondari Maneromango waliotakiwa kuanzia kufanya mitihani yao
Machi 27, 2012 shuleni hapo.
Akizungumza katika
mahojiano na Ripota wetu katika shule hiyo iliyopo Kata ya Maneromango,
Wilaya ya Kisarawe mkoani Pwani,Mwalimu wa taaluma wa shule hiyo, Jonas
Buheruko alisema ofisi yake imebaini utoro huo baada ya kukusanya taarifa
kutoka vidato vyote.
Akifafanua alisema
hali hiyo ya utoro na hasa wanafunzi kukimbia mitihani hujitokeza mara kwa
mara jambo ambalo limekuwa miongoni mwa vikwazo vya shule hiyo kufanya vizuri
kitaaluma.
Alisema taarifa zilizokusanywa
siku ya kwanza kuanza kwa mitihani hiyo,Machi 27 mwaka huu, zimebaini kidato
cha nne ndiyo wanaoongoza kwa utoro wa mitihani kwani kati ya wanafunzi
106 waliotakiwa kuanza kufanya mitihani hiyo ya majaribio ni 45 pekee
walifanya huku 65 wakiingia mitini.
"Taarifa zangu
nilizokusanya baada ya kuanza tu kwa mitihani zinaonesha kidato cha kwanza
wametoroka wanafunzi 10 kati ya 81, kidato cha pili wametoroka 31 kati ya
103, kidato cha tatu wametoroka 53 kati ya 93 waliotakiwa kuanza kufanya
mitihani hiyo," alisema Mwalimu Buheruko.
Hata hivyo alisema
kitendo cha utoro wa mithani shuleni hapo sasa kinaendelea kuwa sugu licha
ya walimu kufanya jitihada za kuwafuatilia wanafunzi na kutoa adhabu
mbalimbali kulingana na taratibu za shule.
Aidha aliongeza mwaka
2011 wanafunzi 34 wa kidato cha nne kati ya 85 walikimbia kufanya mtihani
wa majaribio wa Wilaya shule hapo jambo ambalo linawakatisha tamaa walimu
katika utoaji wa elimu shuleni hapo.
"Wamekuwa
wakikimbia mitihani mara nyingi...tunawapa adhabu lakini wapo radhi
kufuraia adhabu unayowapa kuliko kuja kufanya mitihani...wakati mwingine
tunapozidiwa tumekuwa tukipeleka majina ya watoro kwa Mwenyekiti wa Kijiji
na Ofisa Mtendaji wa Kata lakini bado hatujaweza kudhibiti utoro huu,"
aliongeza mwalimu Buheruko.
Akizungumzia hali
hiyo, Mratibu wa Elimu Kata ya Maneromango, Nicolaus Lemma amesema
wamekuwa wakiwaita mara kadhaa wazazi wa wanafunzi na kuwashtaki pale
inapobainika wanachangia utoro wa watoto wao, ila tatizo hilo si kwa
sekondari pekee bali hata shule za msingi eneo hilo.


0 Comments