Tunamzomea Bocco kwa faida ya nani?
KATIKA
mechi 18 alizoanza msimu huu, mshambuliaji wa Azam FC, John ‘Adebayor’
Bocco, amepachika wavuni mabao 15 katika Ligi Kuu ya Tanzania.
Hii
ni rekodi bora zaidi kwa mshambuliaji wa Kitanzania msimu huu. Lakini,
misimu miwili iliyopita, Bocco alifunga mabao 12 na 14 kwenye msimu
mmoja na kuwa miongoni mwa wafungaji bora wa msimu uliopita.
Mwanzoni
mwa mwaka huu, Bocco –ambaye ndiyo kwanza ana umri wa miaka 21 tu,
alikuwa mfungaji bora wa Kombe la Mapinduzi lililofanyika visiwani
Zanzibar ambako timu yake ilitwaa kombe. Labda hapo bado hujapata picha
kamili kumhusu huyu mchezaji!
Katika
raundi ya kwanza ya Ligi Kuu msimu huu, Azam ilimleta nchini
mshambuliaji hatari kutoka Ghana, Abdul Wahab Yahya, kucheza katika timu
yao.
Kwa
wasiofahamu, Wahab alikuwa mfungaji bora namba tatu katika Ligi Kuu ya
Ghana msimu uliopita. Hata hivyo, raia huyo wa Ghana hakufua dafu kwa
Bocco na ndiyo maana amerejea kwao baada ya kukosa namba katika kikosi
cha kwanza.
Michael
Kipre Tchetche, mshambuliaji mahiri kutoka Ivory Coast aliyekuwa
mfungaji bora wa Kombe la CECAFA mwaka juzi, anacheza timu moja na Bocco
lakini hajafikia nusu ya mabao ambayo Mtanzania huyo amefunga msimu
huu.
Bocco
amefunga karibu katika mechi zote anazocheza dhidi ya vigogo wa soka
Tanzania, yaani Simba na Yanga. Bocco alifunga pia katika fainali ya
Kombe la Mapinduzi wakati timu yake ikitwaa kombe.
Sifa moja kubwa ya mchezaji mkubwa ni kwamba huwa anafanya mambo makubwa katika mechi kubwa. Huyu kijana tayari ana sifa hiyo.
Naomba
nirudie, Bocco ndiyo kwanza ana umri wa miaka 21 tu. Hata hivyo,
nimesikitishwa na vitendo ambavyo kijana huyu amekuwa akifanyiwa na wale
wanaojiita mashabiki wa soka hapa nchini.
Kwa
wanaokwenda Uwanja wa Taifa kushuhudia mechi za timu ya taifa, watakuwa
wamebaini namna mashabiki wa soka wanavyompa wakati mgumu kijana huyu
kulitumikia taifa lake.
Bocco
amekuwa akizomewa na mashabiki katika karibu mechi zote ambazo amepewa
nafasi na walimu kucheza. Matokeo yake, kiwango chake katika timu ya
taifa kimekuwa kikiathirika.
Na hapa ndipo linapokuja swali langu kubwa la makala hii ya leo, Watanzania wanamzomea Bocco kwa faida ya nani?
Bocco ni tumaini la Tanzania
Kwa
maoni yangu, Bocco ni tumaini la Tanzania kwa miaka walau 10 ijayo kama
atatumiwa vizuri. Hao wanaomzomea Bocco, wana mbadala wake? Je, ni
Watanzania kweli? Kama ni Watanzania; je, uzalendo wao umejitosheleza
mioyoni mwao?
Kocha
Mkuu wa Taifa Stars, Jan Borge Poulsen, amekuwa akilalamika kwamba
tatizo kubwa la Tanzania kwa sasa ni kukosa mshambuliaji wa maana.
Na
hili ndilo tatizo pia alilokuwa nalo mtangulizi wake, Marcio Maximo.
Tanzania haizalishi tena washambuliaji wa kutisha kama ilivyokuwa
zamani.
Kwa
bahati nzuri, kuna vijana watatu wamejitokeza hapa nchini ambao
wanaonyesha kila dalili kuwa watakuja kuwafuta machozi Watanzania katika
muda si mrefu kutoka sasa.
Vijana hao ni Bocco, Mbwana Samatta na Thomas Ulimwengu wote wa TP Mazembe ya DR Congo.
Najua
wako vijana wengi wanaochipukia vizuri katika safu ya ushambuliaji hapa
nchini lakini hawa watatu ni bora zaidi. Nilitarajia Watanzania wawape
moyo vijana hawa lakini badala yake wanazomewa.
Nimemuona
Bocco akifunga magoli magumu katika klabu yake ya Azam, lakini
nimemuona akikosa magoli rahisi wakati akiichezea timu ya taifa. Hii
yote ni kwa sababu ya kukosa kujiamini.
Na
hawezi kujiamini wakati mashabiki wake wanamzomea kuanzia kosa lake la
kwanza katika dakika ya kwanza ya mchezo hadi atakapotolewa. Naomba
nirudie, ndiyo kwanza ana umri wa miaka 21 tu.
Makosa ni darasa kwa Bocco
Watu
wanatarajia nini kutoka kwa kijana wa miaka 21 ambaye ndiyo kwanza
anakua kama mwanasoka? Huu ndiyo umri ambao Bocco anaruhusiwa kufanya
makosa na kujifunza kwayo.
Mashabiki
wa kweli wa soka wanatakiwa kumpa kijana huyu kila aina ya uungwaji
mkono inayohitajika. Uungwaji mkono kwa njia ya mawazo au ushauri na
maelekezo ya kiufundi. Apewe sapoti si kumzomea.
Kwa
maoni yangu, huyu ni mchezaji ambaye anatakiwa kuangaliwa na kuboreshwa
kwa maslahi ya taifa letu hili. Miaka mitatu ijayo ambapo atakuwa
amewiva zaidi kimwili na kiakili, Tanzania itajivunia kuwa na mchezaji
kama yeye.
Lakini,
kama tutaendelea na utaratibu wetu wa kumzomea, taifa letu linaweza
kujikuta limepoteza mchezaji muhimu sana. Katika soka la Tanzania ambapo
wataalamu wa saikolojia ya wachezaji ni kama vile hakuna, ni rahisi
sana kumtoa mchezaji mchezoni.
Kwa
wanaofuatilia soka la Tanzania, watabaini kuwa hiki ni kipindi cha
mpito. Kuna kizazi kinaondoka na kuna kizazi kipya kinaingia.
Kizazi
kipya ni akina Bocco, Samatta, Shomari Kapombe, Jonas Mkude, Hussein
Javu, Mwinyi Kazimoto na wengineo wengi. Hawa wote wanahitaji sapoti kutoka kwa mashabiki na si kuzomewa kila wanapofanya makosa.
Kwa nini Bocco na si wengine?
Kuna
mtakaouliza kwa nini nimetumia mfano wa Bocco pekee wakati kuna vijana
wengi wanachipukia siku hizi. Majibu yangu ni kwamba huyu ndiye
anayeongoza kwa kuzomewa na hili linaniuma kwa sababu ni kijana mwenye
uwezo mkubwa sana.
Kwa
wanaofuatilia soka la Uingereza, watakuwa wamepata habari kuhusu
mchezaji anayeitwa Andrew Alexander Cole (Andy Cole). Huyu ni
mshambuliaji mahiri katika historia ya Ligi Kuu ya England lakini
hakupata mafanikio katika timu yao ya taifa.
Wachambuzi
wanadai kwamba kilichomponza Cole ni kule kuzomewa kwake mara kwa mara
na mashabiki kila alipopewa nafasi katika timu yao ya taifa.
Matokeo
yake Cole akawa na sura mbili; kiwembe kwenye ngazi ya klabu lakini
butu anapokuwa timu ya taifa. Bahati nzuri Waingereza walikuwa na Alan
Shearer, Les Ferdinand, Ian Wright na Teddy Sheringham ambao wangeweza
kutumika bila ya wasiwasi wowote kwa vile walikuwa na ama kiwango sawa
na Cole au pengine kumzidi.
Tatizo
ni kwamba, Tanzania hatuna mtu kama Bocco hivi sasa na pengine kwa
miaka mitano ijayo. Habari njema ni kwamba kijana huyu atakuwa hatari
zaidi huko tuendako.
Maana ya urefu wa Bocco
Wachezaji
warefu kama Bocco wana tabia ya kuchelewa kushika kasi kwa sababu ya
maumbo yao. Wanasaikolojia ya soka wanaamini kwamba kadri umri wa
wachezaji wa aina hii unavyoongezeka, ndivyo ubora wao unavyoongezeka
pia.
Kadiri
umri unavyoongezeka, ndivyo wanavyokuwa na busara zaidi, uimara zaidi,
shabaha zaidi na ujanja zaidi. Wanakuwa washambuliaji bora zaidi kuliko
walivyokuwa vijana.
Sasa
kwa nini tunataka kuipoteza bahati hii kwa Bocco? Tunataka kumfaidisha
nani kwa kumzomea au kumfanyia kijana huyu vitendo visivyo vya
kiungwana?

0 Comments